Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezifutia leseni za uendeshaji wa shughuli za kibenki Benki tano ambazo zimeshindwa kukidhi matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo Gavana wa Benki Kuu anayemaliza muda wake amesema kuwa hatua hiyo imefikiwa kufuatia benki hizo kushindwa kutekeleza matakwa ya kisheria yaliyozitaka benki zote za kijamii kuongeza kiwango hicho cha mtaji ili ziweze kujiimarisha licha ya kupewa muda wa kipindi cha miaka mitano ulifikiwa tamati tarehe 31 Juni 2017.
“Maamuzi haya tunayafanya baada ya Benki zote nchini kupewa muda wa miaka mitano na nusu yakuweza kukidhi matakwa ya sheria, lakini mpaka ilipofika tarehe 31 Desemba 2017 jumla ya benki Nane zilishindwa kuongeza mtaji uliohitajika kati ya hizo Benki  Tano zilishindwa kuwasilisha mpango kazi wa kuonyesha namna zitakavyo kuwa endelevu,” alisema Profesa Ndulu.
Profesa Ndulu alizitaja Benki hizo kuwa ni pamoja na Convenant Bank for Women (T) Limited, Efatha Bank Ltd, Njombe Community Bank Ltd, Kagera Famers’ Cooperative Bank Ltd na Meru Community Bank Ltd.
Aliongeza kuwa Benki hizo kuanzia leo tarehe 4 Januari 2018 , Benki hizo zitakuwa chini ya Bodi ya Bima ya Amana ambayo imeteuliwa kuwa mufilisi wa benki hizo kwa mujibu wa sheria.
Aidha Profesa Ndulu alisema kuwa Benki  tatu zimepewa muda wa miezi sita kuwa zimeongeza mitaji yao baada ya kuwa zimewasilisha mikakati yao ya namna zitakavyoweza kuongeza mitaji na kuwa endelevu benki hizo ni pamoja na Kilimanjaro Cooperative Bank Ltd, Tanzania Women’s Bank PLC, Tandahimba Community Bank Ltd.
Katika kutimiza  jukumu la kuhakikisha uimara na uhimilivu wa sekta ya kibenki na kifedha nchini mwaka 2012  Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliongeza kiwango cha chini cha mtaji wa benki za wananchi kuwa shilingi bilioni 2 na kutoa muda wa miaka mitano kwa benki zote nchini kuweza kuwa zimekuza mitaji yao.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top