MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali itamchukulia hatua mtu yeyote atakayejenga katika eneo lisilopata ridhaa ya mamlaka zinazohusika na masuala ya ujenzi, ardhi na mipango miji na vijiji.

Alitoa tahadhari hiyo wakati alipofanya ziara ya kulikagua eneo linalotarajiwa kujengwa hospitali ya rufaa huko Binguni wilaya ya Kati.

Alisema imejitokeza tabia ya muhali inayofanywa na baadhi ya viongozi wanaopewa jukumu la kusimamia sheria na taratibu za serikali kiasi kwamba watu huamua kuchukuwa sheria mikononi mwao.

Alisema serikali imeamua kudhibiti ujenzi holela katika maeneo mbalimbali hasa yale yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo na miradi mengine ya maendeleo.

Aliuagiza uongozi wa wizara ya Afya kuhakikisha kwamba eneo hilo lililotengwa na serikali kwa ajili ya mradi wa ujenzi hospitali linakuwa katika udhibiti unaostahiki.

Akitoa maelezo, Mkurugenzi Idara ya Tiba Dk. Mohamed Dahoma alisema eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 83 liko kwenye udhibiti wa wizara ya Afya kwa ajili ya mpango wa baadae wa ujenzi wa hospitali ya rufaa.

Dk. Dahoma alimueleza Balozi Seif kwamba wizara ya Afya kupitia wataalamu wa uchambuzi yakinifu inaendelea na uhakiki wa eneo hilo kwa lengo la kufanya michoro itakayotoa muelekeo wa uendelezaji wa mradi huo.

Alisema mradi huo mkubwa utatekelezwa kwa awamu tatu na umepangwa kuwa na kitengo cha mafunzo, hospitali ya kulazwa wagonjwa baina ya 200 na 300, nyumba za wafanyakazi na majengo ya utawala.
NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top