Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ katika Awamu ya Sita ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ndugu Said Abdullah Natepe aliyefariki Dunia jana amezikwa leo jioni Kijijini kwao Mwakaje Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa Mjini Magharibi.
Nd. Said alifariki Dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili Mjini Dar es salaam wakati akipatiwa huduma za Matibabu baada ya kusumbuliwa na Ugonjwa wa Moyo.
Mamia ya Wananchi, Wafanyakazi wa Taasisi za Serikali, zile za Ulinzi walihudhuria Mazishi hayo wakijumuika pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein kwenyemazishi hayo.
Wengine waliohudhuria Mazishi hayo ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Mungano Mh. Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Muungano Dr. Mohamed Gharib Bilal na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Aman Karume.
Marehemu Said Abdullah Natepe alizaliwa Mnamo Tarehe 19 Febuari 1968 ambapo baadae katika makuzi yake alianza kupata Elimu ya Msingi iliyokwenda sambamba na ile ya Madrasa.
Baadae aliendelea na masomo yake ya Sekondari yaliyomuwezesha kupata fursa ya kujiunga na masomo ya elimu ya Juu Nchini Urusi.
Marehemu Said Abdullah Natepe aliajiriwa Ofisi ya Iliyokuwa ya Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Wadhifa wa Afisa Utumishi.
Kutokana na Elimu na Uzalendo aliokuwa nao Ndugu Said katika majukumu yake kwa Umma alimudu vyema nafasi aliyopewa na kumuwezesha kupanda daraja hatua baada ya hatua kwa kuanzia Wadhifa wa Mkurugenzi Afya Wizara ya Afya Zanzibar.
Juhudi zake zilizonekana na hatimae kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Awamu ya Sita.
Marehemu Said Natepe alikuwa Mkarimu, Mcheshi na Mtu wa Watu muda wote wa maisha yake na hata sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake sifa iliyomjengea fursa ya kuteuliwa tena kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Ikulu.
Ndugu Said aliwahi kupata matatizo ya Kiafya kwa muda mrefu ndani ya Utumishi wake wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kufanyiwa upasuaji wa moyo Nchini Afrika Kusini ambapo baadae alipopata nafuu aliendelea na majukumu yake ya Kazi katika Ofisi ya Rais Ikulu.
Marehemu Said Abdullah Natepe aliyefikia umri wa Miaka 50 akiwa bado anaendelea na Utumishi wa Serikali ameacha Kizuka Mmoja na Watoto Watatu
Mwenyezi Mungu alilaze Roho ya Marehemu Said Abdulla Natepe iliyoonja Mauti mahali pema Peponi. Amin.
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment