Mahakama ya wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemuhukumu Ramadhani Shaban (24) mkazi wa mtaa wa Majengo B kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumpata na hatia ya kumbaka mtu mwenye ulemavu wa kuongea ‘Bubu’ na akili mwenye umri wa miaka 15 (jina limehifadhiwa).
Hukumu ya kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi wa mjini Mpanda imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Gasper Luoga baada ya mshitakiwa kukiri kutenda kosa hilo.
Awali katika hati mashtaka, mwendesha mashtaka ambaye ni mwanasheria wa Serikali mkoa wa Katavi, Flaviana Shio alidai mahakamani hapo kuwa, Shabani alitenda kosa hilo Septemba 9 saa 12:00 jioni katika mtaa wa Majengo B.
Alidai siku yatukio mshitakiwa alikwenda kwenye maeneo ya mtaa wa Mji Mwema alikokuwa akiishi mlalamikaji kwa mjomba wake Ernest Chambala na kumpakia kwenye baiskeli yake.
Alidai baada ya kumpakia alikwenda naye hadi kwenye chumba chake alichopanga katika mtaa wa Majengo B na kisha alianza kumbaka mpaka alipomaliza haja yake.
Mwendesha mashtaka huyo alidai baada ya mshitakiwa kumaliza kitendo hicho, mlemavu huyo wa kuongea na akili alitoka nje na kuanza kuwaonyesha watu ishara kuwa amebakwa.
Alidai mjomba wa mlalamikaji huyo alianza kumsaka mtu aliyehusika kutenda kitendo cha kumbaka mpwa wake ambaye alimwongoza hadi kwenye nyumba na chumba alichofanyiwa kitendo hicho kibaya.
Alidai majirani wa nyumba hiyo walipoulizwa kama walimwona mlemavu huyo akiingizwa kwenye chumba cha mshitakiwa walithibitisha kumwona akiingia naye ndani.
Mshitakiwa baada ya kukamatwa alichukiliwa na kupelekwa kituo cha polisi cha Mpanda na katika maelezo yake alikiri kutenda kosa la kumbaka mlemavu huyo na taarifa za daktari zilionyesha alikuwa ameingiliwa na mwanaume.
Baada ya mshitakiwa kukiri kosa, Hakimu Luoga alimweleza Mahakama imemtia hatiani hivyo kama anayo sababu yoyote ya msingi ya kuishawishi mahakama impunguzie adhabu anapewa nafasi ya kujitetea .
Katika utetezi wake aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa mama yake mzazi anamtegemea kwani baba yake ameishafarikidunia.
Hakimu Luoga baada ya kusikiliza utetezi huo, aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa amepatikana na hatia kwa mujibu wa kifungu cha sheria Namba 130 (1) (2) e na 131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.
Hivyo, alimuhukumu Shabani kwenda kutumikia jela kifungo cha miaka 30.
Chanzo Mwananchi
Post a Comment