Mkuu wa Takwimu za Bei Zanzibar Khamis Abdul-rahman Msham kushoto akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari kuhusiana na Takwimu za Bei ambapo zimeonekana kushuka kutoka asilimia 5.2 kwa mwezi wa January hadi asilimia 4.8 kwa February hafla iliofanyika Ofisini kwake Mazizini Mjini Zanzibar.kulia ni Mchumi kutoka Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka Dk,Suleiman Simai Msaraka.
PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.

Kasi ya mfumuko wa bei wa Zanzibar kwa mwaka uliomalizikia Februari 2018, imeshuka na kufikia asilimia 4.8 ikilinganishwa na asilimia 5.2 mwezi Januari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Bei Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Khamis Abrahman Msham, alisema mfumko wa bei za vyakula na vinywaji visivyokuwa na vilevi ulishuka ambapo ulifikia asilimia 1.3 ikilinganishwa na 1.8 kwa mwezi huo.

Alisema kwa jumla faharisi za bei ziliongezeka hadi 105.1 mwezi Februari 2018 ikilinganishwa na 100.2 zilizorikodiwa mwezi Februari 2017.

Alisema kiwango cha mfumuko wa bei kwa vyakula kwa mwaka kilipungua hadi asilimia 1.2 kwa mwaka uliomalizikia Februari 2018 ikilinganishwa na asilimia 1.7 kwa mwaka uliomalizika Januari 2018.

Faharisi za bei kwa vyakula ziliongezeka hadi 101.4 mwezi Februari 2018 ikilinganishwa na 100.2 mwezi Februari 2017, wakati fararisi za bei kwa jumla kwa bidhaa zisizokuwa za vilevi ziliongezeka hadi 107.8 mwezi Februari 2018 ikilinganishwa na 100.3 mwezi Februari 2017.

Kwa upande wa bidhaa zisizokuwa za vyakula, mfumko wa bei ulipungua hadi asilimia 7.6 mwezi Februari ikilinganishwa na asilimia 7.7 mwezi Januari 2018.

Bidhaa zinachangia kupungua kwa kiwango cha mfumko wa bei kwa mwaka zilikuwa unga wa mahindi (25.3%), ndizi za mtwike (8.1%), mkono mmoja (10.9%), Sukari (3.5%) na saruji (4.6%).

Mhadhiri wa Uchumi, Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Chwaka, Dk. Suleiman Simai Msaraka, alisema kwa ujumla hali ya uchumi sio mbaya na inakwenda katika mazingira yanakubalika kiuchumi.

“Tunakwenda vizuri, hali ya kupanda na kushuka kwa mfumko wa bei ni ya kawaida kiuchumi,” alisema.

Akizungumzia upatikanaji wa mafuta, Mchumi Mkuu na Ofisa Masoko wa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Omar Ali Yussuf, alisema, hali hivi sasa ipo vizuri baada ya wiki mbili za upungufu wa nishati hiyo.

Alisema ZURA ilichukua hatua mbali mbali kukabiliana na tatizo hilo  na matarajio ni kuendelea kwa upatikanaji wa nishati hiyo.

“Matumizi ya mafuta hivi sasa yapo juu na  kunapotokea upungufu hali kidogo inakuwa sio nzuri.Ni karibu ongezeko la asilimia 36  ikilinganisha na miaka miwili iliyopita,” alisema.

Kwa sasa Zanzibar inatumia lita milioni 12 kwa mwezi ambapo kwa siku matumizi ya petroli ni lita 180,000 na dizeli lita 160,000.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top