Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein leo amewaapisha Mawaziri pamoja na baadhi ya viongozi aliowateua jana kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hafla hiyo ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali akiwamo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,Said Hassan Said, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu , Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Wakuu wa Vikosi vya SMZ, Washauri wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Mawaziri walioapishwa ni Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salim Ali, Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk Sira Ubwa Mamboya.

Wengine ni Waziri wa Afya, Hamad Rashid Mohamed, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Rashid Ali Juma, Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Maudline Cyrus Castico.

 Manaibu waliapishwa ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Juma Makungu Juma, Naibu Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Choum Kombo Khamis, Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Shadia Mohamed Suleiman, Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk Makame Ali Ussi, Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Hassan Khamis Hafidh.

Dk Shein pia aliwaapisha Wakuu wa Wilaya aliowateua hapo juzi ambao ni Issa Juma Ali aliapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Pemba na Rajab Ali Rajab kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Viongozi hao walioapishwa kwa pamoja waliahidi kuendelea kumsaidia Rais Dk Shein katika kuhakikisha Zanzibar inazidi kupata maendeleo kama ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyosema.

“Tunaendeleza kuimarisha mashirikiano ya dhati katika kuwatumikia wananchi, kuleta mabadiliko na kufanya kazi kwa vitendo sambamba na kuendelea kusimamia amani na utulivu uliopo nchini” walisema .

Hatua hiyo imekuja baada ya jana Dk Shein kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mapinduzi kwa kuongeza Wizara moja zaidi na kuwabadilisha Wizara baadhi ya Mawaziri.

Kufuatia mabadiliko hayo, shughuli za Vijana zimehamishiwa katika Wizara mpya ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo shughuli za Mazingira zimehamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na shughuli za Wakala wa Serikali wa Uchapaji zimehamishiwa Wizara mpya ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale.Aidha.

Dk Shein pia amewateua Naibu Mawaziri wapya wawili na kumbadilisha Wizara Naibu Waziri mmoja ambapo kufuatia mabadiliko hayo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa itakuwa na Wizara 14 badala ya 13 za hapo awali .

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top