MWENYEKITI wa kamati ya ardhi na mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma ameeleza kuwa taarifa zilizotolewa na mjumbe mmoja wa kamati hiyo juu ya kukosekana kwa huduma muhimu kwa viongozi wastaafu nchini hazina ukweli.

Akimtaja mjume huyo, Hamza alisema Mohammed Hasanali Raza hakushiriki katika vikao vya kamati hiyo wakati masuala hayo yakijadiliwa kwa sababu tofauti zikiwemo za ugonjwa uliokuwa ukimsubua kwa muda mrefu.



Akitoa majumuisho ya kamati hiyo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea katika ukumbi wa baraza hilo, Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Hamza alisema malalamiko ya mjumbe huyo hayakuwa na msingi kutokana na mjumbe huyo kutokuwepo wakati masuala hayo yakijadiliwa.

“Raza hakuwepo kwa muda mrefu wakati kamati ikiendelea na shughuli zake, inashangaza kuibuka na hoja ambayo inaibua changamoto ambazo zinaweza kuligawa baraza na kamati.  Ni kauli za kujifurahisha na kujitafutia umaarufu”,  alisema Hamza.

Aidha aliongeza kwamba hoja na malalamiko za mjumbe huyo ingelikuwa busara zikajadiliwa katika vikao vya kamati kabla ya kuibuka ndani ya ukumbi wa baraza.

Hamza alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekuwa ikitenga fungu maalum la kuwahudumia viongozi wakuu wastaafu kutokana na mchango mkubwa walioutoa kwa taifa wakati wakiwepo madarakani.

“Inashangaza kuona Raza ameibuka na hoja ambayo haikuwa katika hoja za kamati, hoja ambayo inaweza kuleta migongano na mizozo kati ya wananchi na serikali”, alisema Hamza.

Mwenyekiti huyo alifahamisha kwamba hoja aliyoitoa Raza ni hoja na mawazo yake binafsi na sio maagizo wala mchango wa kamati hiyo.

Hamza aliwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kufanya utafiti na kuwa makini wakati wanapowasilisha hoja na miswada wakati wa vikao vya baraza hilo ili mawazo yao yaweze kuleta tija kwa taifa.

Alisema wajumbe wanapoibuka na hoja ambazo hazifanyiwi tafiti zinasababisha mizozo na migongano kwa wananchi ambao wanawategemea wawakilishi ikiwa ni miongoni mwa mihimili mikuu ya kuendesha nchi.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top