BARABARA ya Ole-Kengeja yenye urefu wa kilomita 35 ambayo ilianza kujengwa mwaka 2014, itakamilika kwa kiwango cha lami mwaka 2020.

Hayo yalifahamika wakati Mshauri Rais  wa Zanzibar Pemba, Dk. Mauwa Abedi Daftari, alipofanya ziara ya kuitembelea barabara hiyo na nyengine kwenye ziara yake ya siku moja.

Mhandisi ujenzi wa barabara hiyo, Amin Khalid Abdalla, alisema tayari kilomita saba zimewekewa lami, huku kilomita nne zikiwa zimekamilika kwa kiwango cha kifusi.

Aidha alisema kilomita 11 zinaendelea na usafi huku kilomita nyengine zilizobakia zikiwa hazijafikiwa kwa hatua yoyote.

Alisema mradi huo unajengwa kwa ufadhili wa Jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi (OPEC) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Kama kila kitu kitakwenda kama tulivyokipanga basi mwaka 2020 tutaikabidhi kwa serikali ikiwa na lami kwa kilomita zote 35, kuanzia Ole hadi Kengeja,” alisema.

Aidha alisema wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha wananchi wote waliopata athari iwe ya nyumba au mali nyengine ili kupisha ujenzi wa mradi huo, wanafidiwa kama ilivyofanywa sehemu nyengine.

Kwa upande wake, Dk. Daftari, aliiomba wizara hiyo kuhakikisha wanayafanyia matengenezo ya dharura kwa maeneo yenye usumbufu wakati wa mvua.

Alisema mvua zinakaribia kunyesha na inawezekana yapo maeneo wananchi wanayatumia kwa shughuli zao, kwa hivyo lazima yapewe kipaumbele kutengenezwa.

“Yapo maeneo ambayo hayana sehemu nyengine ya kukimbilia na pengine yametibuliwa wakati wa usafishaji, sasa lazima muyaweke mawe ili yapitike wakati wowote,”alisema.

Hata hivyo, aliipongeza wizara kwa juhudi inazochukua katika kutekeleza maagizo ya serikali ya ujenzi wa barabara kadhaa.

Alisema kwa sasa wananchi wa Ngomeni watasafirisha mazao yao bila usumbufu kwa vile barabara yao yenye urefu wa kilomita 3.5 imeanza kutiwa lami baridi.

Mapema Ofisa Mdhamini wizara ya mawasiliano, Hamad Ahmed Baucha, alisema wanafanya kazi hiyo kwa juhudi kubwa.

Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa watendaji wa wizara, ili kukamilisha kwa wakati mradi huo.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top