SERIKALI ya wilaya ya Kati kwa kushirikiana na Kamisheni ya Kazi, Ajira na Usalama wa Afya kazini, imeahidi kuyashughulikia malalamiko ya wafanyakazi wanaoshughulika na utafiti wa gesi na mafuta Zanzibar ndani ya wiki mbili.

Mkuu wa wilaya ya Kati, Mashavu Said Sukwa alieleza hayo wakati akizungumza na wafanyakazi zaidi ya 100 walioajiriwa na kampuni ya BGP ya  China waliogoma huko ofisi kwao Marumbi.

Alisema katika kikao hicho kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Ajira pamoja na Mkurugenzi wa Afya kazini walikubaliana kuzifanyia kazi changamoto hizo ili kuona wafanyakazi hao wanapata haki zao zote.

Alisema masuala hayo ni pamoja na  suala la kupata mapumziko kwani haipo katika sheria kuruhusu mfanyakazi kukosa siku ya kupumzika.

Hata hivyo, alisema kwa suala la usalama wa afya kazini litashughulikiwa kwani wafanyakazi wanakuwa na wakati mgumu wanapokuwa katika maeneo ya kazi ikiwemo misituni na kukata visiki hali ambayo usalama wao ni mdogo mno.

Akizungumzia kuhusu suala la chakula, alisema serikali itarudisha mama mtilie katika maeneo hayo ili wafanyakazi hao waweze kupata chakula kama walivyokuwa wakipata awali.

Wakizungumza na Zanzibar Leo, baadhi ya wafanyakazi hao walisema tangu  wameingia makubaliano  na kampuni hiyo miezi miwili sasa, fedha wanazopatiwa kwa ajili ya malazi na chakula hazitoshelezi ukilinganisha na kazi wanazozifanya.

Walisema fedha wanazopewa na kampuni hiyo ni shilingi 6,000 kwa siku pamoja na malazi hali ambayo inawawia vigumu kuendelea na kazi.

Haji Issa Haji ni mmoja wa wafanyakazi hao alisema ni jambo la kusikitisha kuona wameshakaa na uongozi wa kampuni hiyo na kutaka kuongezewa posho hilo lakini hakuna kinachofanyika kwani ukiangalia mahitaji ya malazi na chakula yapo juu kulingana na fedha wanazopatiwa.

“Sisi tunakwenda misituni tokea asubuhi hadi usiku unakula chapati mbili na juisi, hiyo chapati ikifika mud haimo tumboni na kazi zetu unatakiwa kula mara tatu, lakini shilingi 4,000 hazitoshelezi inatubidi tujibane tule mmlo mmoja,” alisema.

Alisema jambo jengine ni kukosa muda wa mapumziko na kwa mujibu wa makubaliano muda wao wa kufanyakazi ni kuanzia saa 1:00 hadi saa 8:00 mchana lakini wanafika muda wa ziada na pesa hawazioni. chanzo Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top