Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM Bara, Pius Msekwa amesema hamahama ya wabunge na madiwani inayosababisha nchi kuingia katika chaguzi ndogo kuziba nafasi zilizoachwa wazi ni tatizo ambalo wakongwe katika siasa, akiwamo yeye waliliona miaka mingi iliyopita.

Amesema akiwa Spika wa Bunge kuanzia Aprili 1994 hadi Desemba 2005, chombo hicho cha dola kiliona tatizo hilo na kupitisha sheria ya kuruhusu chaguzi ndogo kufanyika mara moja ndani ya miaka mitano, lakini ilifutwa na Mahakama kabla ya kuanza kutumika.

“…Tuliokuwepo katika madaraka kwa muda mrefu tuliwahi kuliona hili kwamba uchaguzi mdogo unaigharimu Serikali na walipa kodi pesa nyingi. Kwa hiyo nikiwa Spika wa Bunge tukapitisha sheria kwamba tusifanye uchaguzi mdogo kila unapotokea, tufanye uchaguzi mdogo mara moja katika miaka mitano,” alisema Msekwa.

Msekwa aliyasema hayo jana baada ya kuulizwa na mwandishi wahabari nini mtazamo wake kuhusu wanasiasa, hasa wabunge na madiwani wanaohama vyama vyao na kusababisha chaguzi za mara kwa mara kuziba nafasi zao.

Alisema licha ya wanaohama kuwa na haki ya kufanya hivyo, chaguzi za marudio zinatumia fedha nyingi ambazo ni kodi ya wananchi.

Alibainisha kuwa sheria hiyo ilifutwa baada ya wanaharakati kufungua kesi mahakamani na chombo hicho cha kutafsiri sheria kueleza kuwa hatua hiyo ingewanyima haki wananchi kuwa na wawakilishi bungeni.

Katika kipindi cha mwaka mmoja kumekuwa na wimbi kubwa la wabunge na madiwani kuvihama vyama vyao, huku madiwani sita wa Chadema katika jimbo la Arumeru waliojiunga na CCM wakifungua dimba. Mpaka sasa Chadema kimepoteza madiwani zaidi ya 17 na mbunge mmoja ambao wote wamehamia CCM.

Aliyekuwa mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia naye alihamia CCM huku aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu akihamia Chadema,chanzo Zanzibar 24

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top