ZAIDI ya shilingi milioni 650 zitatarajiwa kutumika kwa ujenzi wa skuli ya biashara Mombasa wilaya ya magharibi ‘B’Unguja.

Fedha hizo zimetolewa na Mwakilishi wa kuteuliwa, Ahmada Yahya Abdul-wakili ambae ni mmiliki wa kampuni ya Shaa Building Contractor.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo iliyofanyika Mazizini,  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alisema ujenzi huo utasaidia kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Alisema  mradi huo utakuwa ni wa ghorofa mbili ambao utajengwa na kampuni ya Shaa na unatarajiwa kukamilika mwaka mmoja na mienzi sita.

Alisema uamuzi uliochukuliwa na Mwakilishi huyo unafaa kupongezwa kwani unadhihirisha jinsi alivyo na kiu ya kusaidia maendeleo ya nchi.

“Ni jambo la kupongezwa kwa mzalendo kujitolea kuiunga mkono serikali katika kuimarisha sekta ya elimu nchini ambayo itasaidia wanafunzi wa skuli hiyo kusoma katika mazingira mazuri,” alisema.

Alisema serikali itamuunga mkono kuhakikisha mradi huo unakamilikwa kwa wakati ili kuwanufaisha walengwa.

Nae Mwakilishi huyo, alisema yupo tayari kufuata masharti atakayopewa na wizira hiyo ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati na unakuwa imara.

Akitoa shukurani kwa niaba ya familia, Zakaria Ahmada Yahya, ambae ni mtoto wa mmiliki wa kampuni ya SHAA,  alisema  atahakikisha ujenzi huo unatekelezwa kama  ilivyokusidiwa ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Kwa upande wa serikali mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu wizara hiyo, Khadija Bakari na upande wa SHAA, ulisainiwa na mmiliki wa kampuni hiyo, Ahmada Yahya Abdul-wakili.

chanzo, Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top