Jeshi la Magereza Tanzania limewasimamisha kazi askari wake kumi na
moja waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya mwanakijiji,
Aloyce Makalla (41) wiki iliyopita.
Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema askari hao
walisimamishwa kazi na Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa
juzi.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, John Masunga alithibitisha
kusimamishwa kwa askari hao lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa
undani zaidi akisisitiza kuwa msemaji wa jeshi hilo ni Kamishna Jenerali
pekee.
Askari waliosimamishwa ambao walishafikishwa katika Mahakama ya
Wilaya ya Korogwe mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Kassim Mkwawa ni Jonas Makere,
Shadrack Lugendo, Lazaro Stephen, Mussa
Zuberi, Ramadhan Yusuf, Robert Alfred, Fhidirish Osmas, Alfonce
Revocatus, Mbesha Naftari, Hamis Msola na Michael Elias.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa hatua ya kuwasimamisha kazi askari hao
imechukuliwa ikiwa ni kupisha vyombo vya sheria kufanya kazi yake kwa
uhuru zaidi na kwamba hatima yao itategemea uamuzi wa mahakama hiyo.
Askari hao wa Wilaya ya Korogwe walifikishwa katika mahakama hiyo
wakikabiliwa na shtaka la kumuua, Makalla, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha
Kerenge wilayani humo.
Ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria mwandamizi wa Serikali,
Saraji Iboru kuwa Januari 22 saa 9.30 katika kitongoji cha Mapangoni
Kijiji cha Kerenge, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua mwanakijiji huyo.
Iboru ambaye alikuwa akisaidiana na mwendesha mashtaka kiongozi,
Shosa Naiman alidai kwamba siku ya tukio, washtakiwa hao walikwenda
nyumbani kwa Makalla wakimtuhumu kwamba Januari 15 alimjeruhi askari
mwenzao aitwaye Sajenti Stephen.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama
hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji. Hakimu
Mkwawa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 15 itakapotajwa tena.
chanzo, zanzibar 24
chanzo, zanzibar 24
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment