Hatimaye mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe ametuliza mtifuano ulioibuka miongoni mwa wanachama wake baada ya
waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kufanya kikao cha faragha na Rais
John Magufuli.
Pia mwenyekiti huyo wa chama hicho kikuu
cha upinzani amesema Chadema haitakubali kuchonganishwa kutokana na
kikao hicho cha viongozi hao wawili.
Mbowe alisema hayo jana baada ya kufanya
mazungumzo na Lowassa, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kupata
taarifa ya kikao chake na Rais kilichofanyika Jumanne iliyopita Ikulu,
Dar es Salaam.
Tangu Ikulu itoe taarifa ya mazungumzo
ya Lowassa na Rais, viongozi wa Chadema wamepokea suala hilo kwa hisia
tofauti, wengi wakimkosoa mbunge huyo wa zamani wa Monduli kwa kusifia
juhudi za Rais Magufuli bila ya kueleza kasoro za Serikali ya Awamu ya
Tano katika kushughulikia demokrasia, uhuru wa habari, mikutano ya
hadhara na masaibu wanayokabiliana nayo viongozi wa upinzani dhidi ya
vyombo vya dola.
Aboubakary Liongo, ambaye ni msemaji wa
Lowassa, alieleza jana kwamba waziri huyo mkuu wa zamani alifanya
mazungumzo na Mbowe kwa lengo la kumpa mrejesho ya kile kilichojiri
Ikulu.
Baada ya taarifa hiyo ya Liongo, Mwananchi iliwasiliana na Mbowe ambaye alithibitisha kuwapo kwa mazungumzo hayo na Lowassa.
“Ni kweli nilikutana na Mheshimiwa
Lowassa na tulizungumza, lakini siwezi kutoa kila kitu. Tulichozungumza
si kwa public (watu wote), lakini muda ukifika kama itahitajika
tutafanya hivyo,” alisema Mbowe.
“Ieleweke kwamba, Ikulu walitoa taarifa
ya dakika tano waliyoona wao inafaa. Kama wanataka watoe mazungumzo yote
ya zaidi ya saa moja na nusu waliyofanya, si kuchagua kipi kiende na
kipi kisiende kwa masilahi yao.
“Kama Ikulu inataka iweke full text
(taarifa yote) ya mazungumzo, si kutoa vitu nusunusu kwa masilahi yao.
Kama wanataka kumchonganisha (Lowassa) na wenzie wameshindwa.”
Hata hivyo, Mbowe hakueleza kama alikuwa
na taarifa za kikao cha Lowassa na Rais baada ya kuulizwa na Mwananchi,
badala yake alijibu swali jingine la kipi kitarajiwe. “Kama nilivyosema
mwanzo, mazungumzo yalikuwa ya faragha, sidhani kama mazungumzo ya
faragha unaweza kuyaweka wazi, ila muda ukifika ikihitajika tutafanya
hivyo.
Tamko la Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, baada ya kukutana na Lowassa linaweza
kutuliza joto ambalo lilikuwa linaonekana kuanza kupanda kutokana na
kila mmoja kutoa kauli yake dhidi ya waziri huyo mkuu wa zamani.
Miongoni mwa waliotoa kauli hizo ni
Mbowe mwenyewe juzi, ambaye alisema sifa alizotoa Lowassa ni maoni yake
binafsi na si msimamo wa Chadema, huku akisema mtu anayemsifu Magufuli
anahitaji “ujasiri wa ziada”.
Mwingine ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema,
Tundu Lissu ambaye alihoji sababu za Lowassa kutomtaarifu Mbowe kuhusu
mwaliko wake Ikulu wakati walikutana siku chache zilizopita.
Pia mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema alihoji sababu za Lowassa kummwagia sifa Rais wakati hali ya
kiuchumi ikiwa mbaya kutokana na biashara kufungwa; wapinzani
wakikamatwa kila mara; mikutano ya hadhara ikiwa imepigwa marufuku;
vyombo vya habari kufungiwa; watu kupotea na Lissu kushambuliwa kwa
risasi.
Hata Umoja wa Vijana wa Chadema
(Bavicha) ulimlaumu Lowassa kwa kupongeza bila ya kuzingatia masuala
mengine yanayoendelea nchini.
Kauli hizo zilionekana kuanza kupandisha
joto Chadema kabla ya Mbowe kukutana na mgombea huyo wa urais mwaka
2015 kupitia Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa na
kuzungumza.
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment