Azam FC imeibuka mshindi wa michuano ya Mapinduzi CUP iliyomalizika usiku wa jana visiwani Zanzibar baada ya kuifunga URA FC ya Uganda kwa jumla ya penati 4-3.

Mchezo huo umelazimika kuingia katika hatua ya penati baada ya kumaliza dakika 90 kwa timu hizo kwenda suluhu.

Katika hatua ya penati, mlinda mlango wa Azam, FC, Razak Abalora ‘Mikono Mia Mia’ ameweza kuonyesha uwezo mkubwa baada ya kupangua mikwaju miwili iliyopigwa na wachezaji wa URA FC. Lakini pia, mlinda mlango wa URA FC aliweza kupangua penati moja.

Azam imeshinda kombe hilo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kulitwaa mwaka jana.
Katika mchezo huo wa fainali, mlinda mlango wa Azam FC, Razak Abalora amechaguliwa kuwa mchezaji bora.

Azam FC wamekutana na URA FC kwa mara ya pili na kufanikiwa kulipiza kisasi ambao walikutana awali katika mchezo wa Kundi A  Januari 5, 2018 ambao watoza kodi wa Uganda walishinda 1-0.
URA FC alitinga hatua ya fainali baada ya kuing’oa Yanga kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90, wakati bao pekee la Shaaban Iddi Chilunda lilitosha kuipeleka Azam FC fainali kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Singida United.

Jumla ya timu 11 zilishiriki michuano ya mwaka huu ambazo ni URA, Jamhuri, Mwenge, Azam na Simba zilizokuwa Kundi A na Zimamoto, Mlandege, Yanga, JKU, Taifa Jan’gombe na Singida United zilizokuwa Kundi B. Zanzibar 24

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top