Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa pamoja na jitihada za Serikali inazochukua katika kuimarisha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama, bado mahitaji ya maji ni makubwa.

 

Dk Shein aliyasema hayo katika maadhimisho ya kilele cha miaka 54 ya Mapinduzi Zanzibar sherehe ambazo zimefanyika juzi katika uwanja wa Amaan Mjini Unguja.

 

Alisema jumla ya lita za maji milioni 234.45 zinahitajika kila siku kwa Unguja na Pemba, ambapo uzalishaji kwa siku ni lita milioni 162.82 sawa na asilimia 67 ya upatikanaji wa maji safi na salama.  Kwa upande wa Mkoa wa Mjini Magharibi upatikanaji wa maji ni asilimia 63, Mkoa wa Kaskazini Unguja asilimia 48 na Mkoa wa Kusini Unguja asilimia 50. Kwa upande wa Pemba Mkoa wa Kaskazini asilimia 83 na Kusini asilimia 87.

 

Katika kutekeleza Mradi wa Maji wa Mkoa wa Mjini Magharibi kutokana na mkopo wa US$ 23.673 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB),  visima 9 vipya vimeshachimbwa na visima 23 vya zamani vimefanyiwa matengenezo.  Mabomba yenye urefu wa kilomita 68 yatalazwa na ujenzi wa matangi utafanywa. Mradi huu utatekelezwa  na Kampuni ya STECOL ya China na kumalizika mwezi Aprili, 2019. Kumalizika kwa Mradi huu kutaongeza upatikanaji wa maji safi na salama  kutoka lita milioni 67 na kufikia lita milioni 81, sawa na ongezeko la asilimia 20.9.

 

Alisema Kampuni ya CRUCS kutoka India inasimamia mradi wa maji, wenye thamani ya mkopo wa US$ milioni 92 ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya  India. Kampuni hiyo, tayari  imeanza maandalizi ya mradi huo kwa kufanya upembuzi yakinifu. Maeneo yatakayofaidika na Mradi huo ni Wilaya ya Magharibi A na B.

 

Kadhalika, Mradi wa maji unaotekelezwa na Kampuni ya “First Highway Engineering” ya China kwa ajili ya vijiji vya Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja, umekamilika Disemba, 2017.

 

Kuhusu visima 150 vilivyochimbwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba, kwa msaada wa Serikali ya Ras Al Khaimah, visima 26 tayari vinatoa maji na yanatumika na visima 14 viliendelea kutayarishwa, katika mwaka 2017.

 

Katika mwaka 2017, Serikali iliendeleza mazungumzo na   Kampuni ya RAK Gas ya Ras Al Khaimah, kwa madhumuni ya kuanza kazi ya utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia.  Awamu ya Kwanza ya utafiti huo ilifanywa mwezi wa Machi, 2017 kwa kutumia ndege ya Kampuni ya “Bell Geospace Enterprises” ya Uingereza iliokabidhiwa kuifanya kazi hio.  Awamu ya pili ya utafiti huo ilifanywa kuanzia tarehe 27 Oktoba, 2017 na Kampuni ya BGP Explorer ya China.  Utafiti huu kwenye awamu ya pili ulihusika katika miamba iliopo kwenye maeneo ya bahari.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top