Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hasan, amesema serikali imezifutia usajili meli mbili  zilizokamatwa zikiwa na shehena ya dawa za kulevya na silaha.

 

Amesema meli hizo zilisajiliwa chini ya mamlaka ya usajili wa usafiri wa baharini, lakini hata hivyo zilisajiliwa kinyume na sheria, “Tanzania haihusiki na shehena za silaha wala dawa za kulevya zilizokamatwa ndani ya meli hizo, bali ilitoa usajili wa meli hizo chini ya mamlaka za usajili ambao ni utaratibu wa kawaida wa kimataifa wa kusajili meli duniani, kwa hiyo kufuatia tukio hilo, tumezifutia usajili meli zote mbili, usajili ulitolewa chini ya taasisi ambayo ilishanyimwa kibali cha kusajili meli, na sasa meli zote zimeshusha bendera ya Tanzania ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa”, amesema Mhe. Samia.

 

Meli hizo zenye namba za usajili IMO 6828753 ikiwa na kilo 1600 za dawa za kulevya kutoka Jamhuri ya Dominika, na nyingine yenye namba IMO 7614966 iliyokamwa ikiwa na silaha zilizokuwa zikisafirishwa kwenda Libya kinyume na sheria za kimataifa, zilikamatwa Desemba, 2017.

 

Sambamba na hilo serikali imesema kuanzia sasa mamlaka husika inapitia taarifa za meli zote zilizosajiliwa nchini ili kuhakiki taarifa zake, na kutoa mapendekezo ya ushauri kwa serikali.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top